Katika kumkomboa mkulima,
mkoa wa Katavi umeanzisha na kusimamia ipasavyo Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ili
kumpatia bei nzuri na kuondoa mnyororo wa mtu wa kati aliyekuwa akinunua mazao
ya wakulima kwa bei ya chini na kujipatia faida kubwa. Mfumo huu umekuwa
ukitekelezwa kupitia masoko ya wazi na soko la bidhaa (TMX).
Akizungumza katika mahojiano
maalum juzi, Juni 16, 2020 mjini Mpanda, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Juma
Homera, amesema kuwa mkoa wa Katavi umedhamiria kuimarisha masoko ya mazao ya
wakulima ili yaweze kuwapatia bei nzuri na kuwezesha kuinua maisha ya mkulima
mmoja mmoja na uchumi wa mkoa kwa ujumla.
“Katika kuimarisha kilimo na
masoko bora, kwa ajili ya kumkomboa mkulima wa mkoa wa Katavi tuameanzisha
Stakabadhi ya Mazao Ghalani ambayo inaendelea kufanya vizuri sana katika mkoa
wetu wa Katavi kwa lengo la kukata mnyororo wa mtu wa kati ambaye anakuwa kama
dalali katika masoko ya mkulima,” alisema Mhe. Homera.
Mauzo ya Ufuta kwa Vyama vya
Ushirika kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala umewezesha jumla ya kilo
1,370,718 kuuzwa katika minada mitatu (3) iliyofanyika mkoani Katavi msimu huu.
Kutokana na mauzo hayo, Shilingi 2,767,200 zililipwa na makampuni yaliyoshiriki
kwenye minada hiyo. Kati ya fedha hizo wakulima walilipwa Shilingi
2,555,511,910 kupitia akaunti zao za benki.
![]() |
Moja ya ghala la kuhifadhia mazao lililojengwa na chama cha ushirika cha Nsimbo AMCOS kilichopo Wilaya ya Nsimbo, mkoani Katavi
Aidha, katika fedha hizo jumla ya Shilingi 82,243,080 zimeingia katika Halmashauri za mkoa wa Katavi kama ushuru ambazo zitatumika katika kuimarisha miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo hayo.
Akizungumzia kuhusu umuhimu wa
Ushirika, Mkuu wa Mkoa wa Katavi amesema kuwa viongozi wote wa mkoa huo
wamekuwa wakihimiza wananchi kujiunga katika vyama vya ushirika kwa kuwa ndiyo
moyo wa uchumi wa mwananchi mmoja mmoja katika ngazi zote kuanzia kwenye
vijiji, kata, tarafa, wilaya na mkoa.
![]() |
Mwenyekiti wa Chama cha
Ushirika cha Katumba AMCOS, Azory
Ntondelo akielezea faida walizozipata baada
ya kujenga ghala la kuhifadhia pembejeo na mazao yao wakati wa mauzo.
Kwa upande wake Mrajis
Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Katavi, Kakozi Amri amesema kuwa
kumekuwepo na ushirikiano mkubwa katika usimamizi wa Vyama vya Ushirika kati ya
viongozi wa mkoa, wilaya, Halmashauri. Ambapo ushikiano huo umewezesha
kuongezeka kwa idadi ya vyama, wanchama na idadi ya mazao yanayoshughukiwa na
vyama vya ushirika.