Thursday, June 11, 2020

ONGEZENI NGUVU YA USIMAMIZI KATIKA VYAMA VYA USHIRIKA - DKT. NDIEGE

Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akitoa maelekezo kwa viongozi wa Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo vya Bariadi Teachers SACCOS, ATAPE SACCOS,Bariadi Hospital SACCOS na Roots and Shoots SACCOS


Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege amewataka Maafisa Ushirika nchini kuongeza nguvu ya usimamizi katika Vyama vya Ushirika kwa kuweka mpango wa kuvitembelea Vyama hivyo mara kwa mara na kuangalia shughuli zinazofanyika.
 

Dkt. Ndiege ametoa maelekezo hayo jana Juni 09, 2020 katika Kikao cha pamoja na Maafisa Ushirika wa Wilaya za Bariadi Mji, Bariadi Vijijini na Itilima alichokifanya akiwa kwenye ziara ya siku moja mkoani Simiyu.

“Ni muhimu kuweka usimamizi imara ili kuondoa dhana ya kufanya uchunguzi, ni bora kugundua tatizo kabla halijatokea na kulidhibiti kuliko kusubiri litokee na kuanza kuchukua hatua,” amesema Mrajis wa Vyama vya Ushirika.

Aidha, Dkt. Ndiege amewataka Maafisa Ushirika kufuatilia makusanyo ya Mfuko wa Usimamizi na Ukaguzi kutoka Vyama vya Ushirika ili kupata fedha za kusimamia Vyama hivyo, na amesema kuwa fedha za makusanyo hayo zitaendelea kupelekwa mikoani na wilayani ili kuongeza usimamizi na kuimarisha Ushirika nchini.  

Akizungumzia Mfumo wa Ushirika katika Ununuzi wa mazao mchanganyiko, Dkt. Ndiege amesema mfumo huo haujafanya vizuri katika baadhi ya mikoa kwa kuwa mfumo ulianza katikati ya msimu ambako tayari kulikuwa na mfumo huria katika unuzi wa mazao.

“Kwa sasa Serikali imeshaelekeza mazao mchanganyiko kuuzwa kupitia Vyama vya Ushirika ni muhimu tukajipanga kwa kuwaelimisha wakulima umuhimu na faida ya kuuzia mazao yao kupitia ushirika chini ya mfumo wa Stakabadhi ya Soko Ghalani,” amesema Dkt. Ndiege.

 Katika kikao hicho Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Simiyu, Ibrahim Kadudu kupitia taarifa ya Ushirika ya Mkoa alisema Vyama vya Ushirika vya pamba Mkoani humo vinakabiliwa na changamoto ya malipo ya Ushuru kiasi cha Shilingi bilioni 3.9 na bado wakulima zaidi ya 11,047 wanadai fedha zao za pamba kiasi cha Shilingi bilioni 3.4 kwa msimu uliopita.

Mrajis Msaidizi Mkoa wa Simiyu Ibrahim Kadudu akiwasilisha Taarifa ya Ushirika Mkoa wa Simiyu  kwa Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege 

Katika ziara hiyo ya siku moja mkoani Simiyu, Dkt. Ndiege alikutana pia na viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Simiyu (SIMCU 2018) na kuwataka kuhakikisha muafaka wa mgawanyo wa mali kati ya SIMCU na SHIRECU unafanyika haraka ili kuruhusu uwekazaji katika mali hizo ambazo ni viwanda vya kuchakata pamba vilivyopo Lugulu, Sola na Malampaka.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Dkt. Benson Ndiegwe (wanne kushoto) akiwa pamoja na Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Simiyu, Ibrahim Kadudu na Wajumbe wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Simiyu

“Viwanda hivi vinapaswa kufufuliwa ili vifanye kazi na haviwezi kufufuliwa mpaka mmiliki afahamike; hivyo, ni lazima kuwepo na maridhiano ya mgawanyo wa mali na madeni kati ya SIMCU na SHIRECU,” alisema Mrajis.

Mwenyekiti wa Bodi wa SIMCU, Emanuel Mwerere alisema kuwa makubaliano hayo yanachelewa kwasababu wanachama wa SIMCU waliamua kupitia Mkutano Mkuu kuwa wapo tayari kupokea mali kutoka SHIRECU lakini hawapo tayari kupokea madeni kutoka SHIRECU kwa kuwa viwanda hivyo vimebaki magofu hivyo watapata gharama mara mbili ya kufufua na kulipa madeni hayo.

Aidha, Dkt. Ndiege vilevile alikutana na viongozi wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) vya Bariadi Teachers SACCOS, Simiyu ATAPE SACCOS, Bariadi Afya SACCOS na Roots and Shoots, ambapo alitoa ufafanuzi kuhusu baadhi ya changamoto zinazojitokeza katika usimamizi na uhamasishaji wa maendeleo ya ushirika nchini.


Viongozi wa Vyama vya Ushirika vya Fedha vya Bariadi Teachers SACCOS, ATAPE SACCOS, Bariadi Hospital SACCOS na Roots and Shoots SACCOS

No comments:

Post a Comment