Thursday, July 2, 2020

NAIBU WAZIRI ULEGA ATEMBELEA VYAMA VYA USHIRIKA WA WAFUGAJI MKOANI TANGA

Muheza, Tanga

Naibu Wazir wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega jana Julai 01, 2020 ametembelea Vyama vya Ushirika wa Wafugaji wa ng'ombe wa maziwa katika wilaya ya Muheza mkoani Tanga.

Naibu Waziri Ulega katika ziara hiyo alikabidhi vibebea maziwa (cans) 50 kwa Chama Kikuu cha wafugaji Mkoani Tanga (TDCU) kwa ajili ya ubebaji maziwa.

Naibu Wazir wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akikabidhi vibebea maziwa (cans) 50 kwa Wanaushirika wa Chama Kikuu cha wafugaji Mkoani Tanga (TDCU) kwa ajili ya ubebaji maziwa


Cans hizo zimetolewa na Marafiki wa Maendeleo, Heifer International kupitia program zake kusaidia ukusanyaji wa maziwa kutoka kwa vyama vya msingi vya wafugaji hadi kiwandani Tanga Fresh Ltd kwa Usindikaji ambapo cans hizi zitagawanya kwa vyama vya msingi wanachama wa TDCU.


Aidha, Naibu Waziri Ulega alikabidhi pia gari la kubebea maziwa kwa TDCU ambalo litasaidia kubeba maziwa ya wafugaji. Gari hilo kwa sasa litakuwa katika kituo cha Muheza na lingine linatarajia kufika mwezi Novemba,2020.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akikabidhiwa gari la kubebea maziwa na Bw. Mac wa Heifer International kupitia program zake kusaidia ukusanyaji wa maziwa kutoka kwa vyama vya msingi vya wafugaji hadi kiwandani Tanga Fresh Ltd kwa Usindikaji. 


Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi na wanachama wa Vyama vya Ushirika wa Maziwa mkoani Tanga.


 Naibu Waziri Ulega pia katika ziara hiyo alikuja kujua kuhusu mafanikio na changamoto za mkopo wa TADB kwa mkoa wa Tanga kwa kuwa mkoa huo ndio ulikuwa wa majaribio (pilot) kwa mikopo ya TADB kwa Sekta ya Ufugaji. Kutokana na changamoto alizoelezwa, Mhe. Ulega alielekeza Wataalam wa Sekta Binafsi kukaa na TADB kutoa mwelekeo wa nini kifanyike kwa Mfugaji.


Naibu Wazir wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiwa na Wanaushirika mbele ya gari la ukusanyaji wa maziwa kutoka kwa vyama vya msingi vya wafugaji hadi kiwandani Tanga Fresh Ltd kwaajili ya Usindikaji.




WAKULIMA WATAKIWA KUWA NA VITAMBULISHO - WAZIRI HASUNGA

Chunya, Mbeya

Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga ametoa wito kwa wakulima nchini kuwa na Vitambulisho ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za mkulima kwa urahisi kama vile aina ya kilimo anachofanya, eneo analotoka, mazao anayolima na taarifa nyingine muhimu za utambulisho wake.

Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga, akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi rasmi wa masoko ya minada ya Tumbaku wa mwaka 2020/21 uliofanyika Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya mwishoni mwa wiki iliyopita Juni 26, 2020

Waziri Hasunga aliyasema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa masoko ya minada ya Tumbaku wa mwaka 2020/21 uliofanyika Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya mwishoni mwa wiki iliyopita Juni 26, 2020. Akifungua masoko hayo Waziri alisisitiza kuwa ni muhimu wakulima kuwa na vitambulisho kwani kilimo ni moja ya Sekta muhimu za uchumi wa Taifa letu kutokana na kilimo kuchangia pato la Taifa pamoja na  asilimia 30 ya fedha za kigeni kwa mahitaji ya kibiashara, ajira, chakula, na malighafi za viwandani.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege, akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi rasmi wa masoko ya minada ya Tumbaku wa mwaka 2020/21 uliofanyika Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya mwishoni mwa wiki iliyopita Juni 26, 2020

Katika hotuba ya ufunguzi huo, Waziri alitoa maelekezo kwa maafisa Ugani wafanye kazi zao kwa bidii wakizingatia kuwahudumia wakulima mashambani. Aliongeza kuwa maafisa ugani watumie muda wao mwingi mashambani ambapo ndipo wanapohitajika kutumia taaluma zao kuongeza uzalishaji wa kilimo chenye tija nchini.
“Kila mkulima asajiliwe, ajulikane yuko wapi analima kiasi gani, analima zao gani, analima ukubwa gani wa shamba, kiwango cha mavuno anachopata pamoja na changamoto alizonazo,” alisisitiza Waziri

Aidha, ameitaka Bodi ya Tumbaku nchini kuongeza kasi ya utafutaji wa masoko ya tumbaku inayozalishwa nchini kutokana na changamoto ya kupungua kwa wanunuzi wa zao la tumbaku pamoja na bei ya zao hilo kuendelea kushuka hivi karibuni. Jambo ambalo linasababisha kipato kwa wakulima kuathirika na mapato ya Serikali kupungua.

Mnada wa Tumbaku kwenye ghala la Chama cha msingi Lupa AMCOS

Pamoja na mambo mengine ameagiza Viwanda vya tumbaku visiuzwe bali vifufuliwe ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuendeleza na kuimarisha Uchumi wa viwanda, ambapo viwanda hivyo vitatumia mazao na malighafi za kilimo, kuongeza ajira na kukuza Sekta ya Viwanda.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akizungumza katika uzinduzi huo amesisitiza Vyama vya Ushirika kuendelea kujikita katika kujenga na kuimarisha mitaji yake ya ndani ili kuwa na nguvu zaidi za kiuchumi katika Vyama itakayowezesha kukopesheka vizuri kwa riba nafuu kutoka kwenye taasisi za Kifedha na mabenki.

Dkt. Ndiege alieleza kuwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na Serikali itaendelea kuchukua hatua dhidi ya wale wote watakaobainika kufanya shughuli za ushirika katika vyama bila kufuata taratibu au watumishi watakaokiuka maadili ya utumishi wa Umma, akimalizia kwa kuwaomba wadau kuendelea kutoa ushirikiano.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Wakulima wa Tumbaku (T.C.J.E), Bw. Emmanuel Charahani  katika maelezo yake amesema kuwa baadhi ya changamoto katika kilimo hicho ni kuendelea kuporomoka  kwa bei ya Tumbaku.  Akifafanua kuwa msimu wa 2016/17 wastani wa bei ulikuwa Dola 2.06 lakini msimu huu ambao soko la Tumbaku limefunguliwa bei ya wastani ni Dola 1.60. Hali inayopelekea wanunuzi na wakulima wa Tumbaku kuzidi kupungua na kuiomba Serikali kusaidia kunusuru hali hiyo kwa kutafuta wanunuzi zaidi wa Tumbaku.

Charahani amesema matarajio ya kitaifa ni kuzalisha kilo millioni 57 za tumbaku ambazo zinauzwa sasa, hii ikiwa imetokana na hali ya hewa mwaka huu ya mvua nyingi zilizosababisha mbolea kupotea ardhini.

Aidha, Mwenyekiti Charahani ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa jinsi inavyoendesha na kusimamia shughuli mbambali za kilimo kwa kutetea maslahi ya watu wanyonge. Ameipongeza pia Serikali kwa kuondoa baadhi ya tozo na kodi za Tumbaku ambazo zitasaidia kujenga hoja zenye nguvu katika kujadiliana bei ya Tumbaku na Wanunuzi.


Thursday, June 18, 2020

TUMEANZISHA MFUMO WA STAKABADHI GHARANI ILI KUMKOMBOA MKULIMA – RC HOMERA

 



Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera akizungumza na Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa huo, Kakozi Amri  pamoja na Wanahabari (hawapo pichani)jinsi ya kuimarisha masoko ya mazao ya wakulima na kusisitiza utumiaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa wakulima wa  mkoa huo ili waweze kufaidika na kuwawezesha kuinua maisha ya mkulima mmoja mmoja na uchumi wa mkoa kwa ujumla

Mpanda, Katavi

Katika kumkomboa mkulima, mkoa wa Katavi umeanzisha na kusimamia ipasavyo Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ili kumpatia bei nzuri na kuondoa mnyororo wa mtu wa kati aliyekuwa akinunua mazao ya wakulima kwa bei ya chini na kujipatia faida kubwa. Mfumo huu umekuwa ukitekelezwa kupitia masoko ya wazi na soko la bidhaa (TMX).

Akizungumza katika mahojiano maalum juzi, Juni 16, 2020 mjini Mpanda, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Juma Homera, amesema kuwa mkoa wa Katavi umedhamiria kuimarisha masoko ya mazao ya wakulima ili yaweze kuwapatia bei nzuri na kuwezesha kuinua maisha ya mkulima mmoja mmoja na uchumi wa mkoa kwa ujumla.

Ununuzi wa Tumbaku ukiendelea katika Ghala la chama cha ushirika cha Mpanda Kati hivi karibuni.

“Katika kuimarisha kilimo na masoko bora, kwa ajili ya kumkomboa mkulima wa mkoa wa Katavi tuameanzisha Stakabadhi ya Mazao Ghalani ambayo inaendelea kufanya vizuri sana katika mkoa wetu wa Katavi kwa lengo la kukata mnyororo wa mtu wa kati ambaye anakuwa kama dalali katika masoko ya mkulima,” alisema Mhe. Homera.

Mauzo ya Ufuta kwa Vyama vya Ushirika kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala umewezesha jumla ya kilo 1,370,718 kuuzwa katika minada mitatu (3) iliyofanyika mkoani Katavi msimu huu. Kutokana na mauzo hayo, Shilingi 2,767,200 zililipwa na makampuni yaliyoshiriki kwenye minada hiyo. Kati ya fedha hizo wakulima walilipwa Shilingi 2,555,511,910 kupitia akaunti zao za benki.

Moja ya ghala la kuhifadhia mazao lililojengwa na chama cha ushirika cha Nsimbo AMCOS kilichopo Wilaya ya Nsimbo, mkoani Katavi

Aidha, katika fedha hizo jumla ya Shilingi 82,243,080 zimeingia katika Halmashauri za mkoa wa Katavi kama ushuru ambazo zitatumika katika kuimarisha miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo hayo.

Akizungumzia kuhusu umuhimu wa Ushirika, Mkuu wa Mkoa wa Katavi amesema kuwa viongozi wote wa mkoa huo wamekuwa wakihimiza wananchi kujiunga katika vyama vya ushirika kwa kuwa ndiyo moyo wa uchumi wa mwananchi mmoja mmoja katika ngazi zote kuanzia kwenye vijiji, kata, tarafa, wilaya na mkoa.

Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Katumba  AMCOS, Azory Ntondelo akielezea faida walizozipata baada  ya kujenga ghala la kuhifadhia pembejeo na mazao yao wakati wa mauzo.


“Katika Mkoa wetu wa Katavi tumekuwa tukisimamia Ushirika kwa kushirikiana na timu yangu yote ya mkoa na wilaya zake ambapo vyama vya aina mbalimbali vimeanzishwa katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi,” amesema Mhe. Homera.

Kwa upande wake Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Katavi, Kakozi Amri amesema kuwa kumekuwepo na ushirikiano mkubwa katika usimamizi wa Vyama vya Ushirika kati ya viongozi wa mkoa, wilaya, Halmashauri. Ambapo ushikiano huo umewezesha kuongezeka kwa idadi ya vyama, wanchama na idadi ya mazao yanayoshughukiwa na vyama vya ushirika.

 “Hapo awali ushirika katika mkoa wa Katavi ulikuwa ukishughulikia zao moja tu la Tumbaku, lakini sasa  vyama vya ushirika katika mkoa wetu vinajihusisha pia na mazao ya Pamba, Ufuta, Korosho na Alizeti. Wakulima wameweza kuongeza kipato kutokana na kuuza mazao haya kwa bei nzuri ikilinganishwa na wakati yalikuwa yanauzwa nje ya mfumo wa ushirika,” amesema Kakozi.


Thursday, June 11, 2020

ONGEZENI NGUVU YA USIMAMIZI KATIKA VYAMA VYA USHIRIKA - DKT. NDIEGE

Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akitoa maelekezo kwa viongozi wa Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo vya Bariadi Teachers SACCOS, ATAPE SACCOS,Bariadi Hospital SACCOS na Roots and Shoots SACCOS


Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege amewataka Maafisa Ushirika nchini kuongeza nguvu ya usimamizi katika Vyama vya Ushirika kwa kuweka mpango wa kuvitembelea Vyama hivyo mara kwa mara na kuangalia shughuli zinazofanyika.
 

Dkt. Ndiege ametoa maelekezo hayo jana Juni 09, 2020 katika Kikao cha pamoja na Maafisa Ushirika wa Wilaya za Bariadi Mji, Bariadi Vijijini na Itilima alichokifanya akiwa kwenye ziara ya siku moja mkoani Simiyu.

“Ni muhimu kuweka usimamizi imara ili kuondoa dhana ya kufanya uchunguzi, ni bora kugundua tatizo kabla halijatokea na kulidhibiti kuliko kusubiri litokee na kuanza kuchukua hatua,” amesema Mrajis wa Vyama vya Ushirika.

Aidha, Dkt. Ndiege amewataka Maafisa Ushirika kufuatilia makusanyo ya Mfuko wa Usimamizi na Ukaguzi kutoka Vyama vya Ushirika ili kupata fedha za kusimamia Vyama hivyo, na amesema kuwa fedha za makusanyo hayo zitaendelea kupelekwa mikoani na wilayani ili kuongeza usimamizi na kuimarisha Ushirika nchini.  

Akizungumzia Mfumo wa Ushirika katika Ununuzi wa mazao mchanganyiko, Dkt. Ndiege amesema mfumo huo haujafanya vizuri katika baadhi ya mikoa kwa kuwa mfumo ulianza katikati ya msimu ambako tayari kulikuwa na mfumo huria katika unuzi wa mazao.

“Kwa sasa Serikali imeshaelekeza mazao mchanganyiko kuuzwa kupitia Vyama vya Ushirika ni muhimu tukajipanga kwa kuwaelimisha wakulima umuhimu na faida ya kuuzia mazao yao kupitia ushirika chini ya mfumo wa Stakabadhi ya Soko Ghalani,” amesema Dkt. Ndiege.

 Katika kikao hicho Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Simiyu, Ibrahim Kadudu kupitia taarifa ya Ushirika ya Mkoa alisema Vyama vya Ushirika vya pamba Mkoani humo vinakabiliwa na changamoto ya malipo ya Ushuru kiasi cha Shilingi bilioni 3.9 na bado wakulima zaidi ya 11,047 wanadai fedha zao za pamba kiasi cha Shilingi bilioni 3.4 kwa msimu uliopita.

Mrajis Msaidizi Mkoa wa Simiyu Ibrahim Kadudu akiwasilisha Taarifa ya Ushirika Mkoa wa Simiyu  kwa Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege 

Katika ziara hiyo ya siku moja mkoani Simiyu, Dkt. Ndiege alikutana pia na viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Simiyu (SIMCU 2018) na kuwataka kuhakikisha muafaka wa mgawanyo wa mali kati ya SIMCU na SHIRECU unafanyika haraka ili kuruhusu uwekazaji katika mali hizo ambazo ni viwanda vya kuchakata pamba vilivyopo Lugulu, Sola na Malampaka.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Dkt. Benson Ndiegwe (wanne kushoto) akiwa pamoja na Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Simiyu, Ibrahim Kadudu na Wajumbe wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Simiyu

“Viwanda hivi vinapaswa kufufuliwa ili vifanye kazi na haviwezi kufufuliwa mpaka mmiliki afahamike; hivyo, ni lazima kuwepo na maridhiano ya mgawanyo wa mali na madeni kati ya SIMCU na SHIRECU,” alisema Mrajis.

Mwenyekiti wa Bodi wa SIMCU, Emanuel Mwerere alisema kuwa makubaliano hayo yanachelewa kwasababu wanachama wa SIMCU waliamua kupitia Mkutano Mkuu kuwa wapo tayari kupokea mali kutoka SHIRECU lakini hawapo tayari kupokea madeni kutoka SHIRECU kwa kuwa viwanda hivyo vimebaki magofu hivyo watapata gharama mara mbili ya kufufua na kulipa madeni hayo.

Aidha, Dkt. Ndiege vilevile alikutana na viongozi wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) vya Bariadi Teachers SACCOS, Simiyu ATAPE SACCOS, Bariadi Afya SACCOS na Roots and Shoots, ambapo alitoa ufafanuzi kuhusu baadhi ya changamoto zinazojitokeza katika usimamizi na uhamasishaji wa maendeleo ya ushirika nchini.


Viongozi wa Vyama vya Ushirika vya Fedha vya Bariadi Teachers SACCOS, ATAPE SACCOS, Bariadi Hospital SACCOS na Roots and Shoots SACCOS

Thursday, June 4, 2020

TUTUMIE USHIRIKA KUPATA MASOKO NA BEI ZA UHAKIKA – NAIBU WAZIRI BASHE

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (wapili kushoto) akiongea kwenye Kikao na Viongozi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Wakulima wa Bonde la Bahi 


Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe ametoa wito kwa Wakulima nchini kutumia Ushirika hususan Mfumo wa Stakabadhi ya Ghala kwa lengo la kupata masoko na bei za uhakika.

Wito huo umetolewa wakati wa Kikao na viongozi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Wakulima wa zao la Mpunga wa Bonde la Bahi, Jumanne Juni03, 2020 alipokuwa katika ziara ya kikazi Wilayani Bahi, mkoani Dodoma.

Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda akiongea na Wanaushirika katika ziara ya Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe kwenye Skimu ya Umwagiliaji ya Wakulima wa zao la Mpunga wa Bonde la Bahi 

Naibu Waziri amesema kuwa Serikali ina dhamira ya dhati ya kumuinua mkulima ili anufaike na kilimo chake. Hivyo, ni vyema wakulima kutumia mifumo ya Ushirika pamoja na vituo vya ukusanyaji mazao katika maeneo yao kwaajili ya urahisi wa kufikisha mazao yao katika maghala ya uuzaji kwaajili ya kupata bei yenye tija itakayopatikana kupitia minada rasmi.

Wanaushirika wa Skimu ya Umwagiliaji ya Wakulima wa zao la Mpunga wa Bonde la Bahi wakiwa katika mkutano na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe

Aidha, Naibu Waziri ametoa agizo kwa watendaji kushirikiana na wakulima wa Skimu ya Bahi kujenga Ofisi ya kuhudumia Skimu hiyo ndani ya eneo la Skimu kwa lengo la kuimarisha huduma kwa wakulima na kuboresha kilimo cha umwagiliaji kinachofanyika hivi sasa. Alisema kuwa ni matazamio ya Serikali kuwa suala hilo litakapoteelezwa kwa ufanisi ni dhahiri kuwa litakuwa ni mfano  wa kuigwa katika maeneo mengine ya Skimu kama hiyo. Aliongeza kuwa Ofisi hiyo itasaidia wakulima kupata huduma kwa urahisi kupitia Afisa Kilimo, Afisa Ushirika pamoja na Wataalamu wengine ambao watapatikana katika miradi hiyo.


Wanaushirika wa Skimu ya Umwagiliaji ya Wakulima wa zao la Mpunga wa Bonde la Bahi wakiongea na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe

Naibu Waziri Bashe amewashauri wakulima kutumia nguvu zao kwa pamoja kuboresha mifumo ya Kilimo waliyonayo ili kuongeza tija na ufanisi zaidi katika Kilimo na amewataka wakulima kuchangia maendeleo yao wenyewe kupitia maamuzi yao ya pamoja ya kuchangia kiasi cha mavuno yao kulingana na uzalishaji wa mkulima na kuuza mazao hayo kwa malengo ya kutatua changamoto zinazowakabili. Changamoto hizo ni pamoja na ujenzi wa maghala, kuboresha na kukarabati miundo mbinu ya Skimu za Kilimo.

“Tunaweza kuamua kuhifadhi kwenye ghala gunia mbili za mazao ya mkulima hiki kikiwa ni wastani wa kwa kiwango cha chini na kwa pamoja tukaamua kuyauza mazao hayo kwa mnada wa uwazi ambapo mapato yatakayopatikana yatusaidie wenyewe kuimarisha kilimo chetu,” alisisitiza Bashe.

Katika Kikao hicho Naibu Waziri amewaagiza Viongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Bahi kutenga maeneo maalum ya uuzaji wa mazao ya wakulima wadogowadogo ili kuwa na urahisi kukutana na wauzaji katika hatua za soko la awali, akisisitiza maeneo hayo kuwa na mizani zilizokaguliwa ili wakulima wauze kwa vipimo sahihi na si vinginevyo.

Wanaushirika wa Skimu ya Umwagiliaji ya Wakulima wa zao la Mpunga wa Bonde la Bahi wakiandaa mazao yao kwaajili ya huhifadhi na kuuza

Mhe. Bashe amewataka Viongozi wa Skimu, Viongozi wa Wilaya ya Bahi kushirikiana kwa pamoja na Wadau wa maendeleo pamoja na taasisi za kifedha kuangalia namna bora ya kuongeza thamani ya mpunga huo kwa kuanzisha  kiwanda chenye kinu cha  kukoboa mpunga na hatimaye kuuza mchele. Jambo ambalo wakulima hao waliliunga mkono kutokana na kuongeza ubora wa thamani na kuongeza kipato kwa wakulima.

Pamoja na mambo mengine, Naibu Waziri ameagiza Watendaji wa Wilaya ya Bahi kwa kushirikiana na Serikali  kuratibu zoezi la kuwatambua wakulima kwa lengo la kuanzisha kanzidata ya wakulima pamoja na upatikanaji wa vitambulisho kwa wakulima wa Bonde la mpunga la Bahi. Akifafanua kuwa Skimu hiyo ikawa ni mfano utakaoendelezwa katika maeneo mengine ili kuongeza tija na ufanisi kwa wakulima.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda amemshukuru Naibu Waziri wa Kilimo kwa kufika katika Wilaya hiyo kuona shughuli mbalimbali za Kilimo zinazoendelea Wilayani hapo. Mkuu huyo alipongeza juhudi zinazoendelea hususani za uimarishaji wa Ushirika kwa mfumo wa Stakabadhi ya ghala ambao unaendelea kutekelezwa Wilayani hapo kipindi hiki ambapo minada ya mazao ikiendelea na wananchi wakinufaika na bei za mauzo za minada hiyo.  


Monday, May 25, 2020

Tume Ya Maendeleo Ya Ushirika Kuja Na Mikakati Ya Kukabiliana Na Upungufu Wa Sukari Nchini


Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini imeweka wazi azma yake ya kusimamia mikakati kazi ya uvunaji wa miwa kwa msimu huu mpya wa mwaka 2020. Hii ikiwa ni hatua ya kukabiliana na upungufu wa bidhaa ya sukari nchini.