Thursday, June 4, 2020

TUTUMIE USHIRIKA KUPATA MASOKO NA BEI ZA UHAKIKA – NAIBU WAZIRI BASHE

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (wapili kushoto) akiongea kwenye Kikao na Viongozi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Wakulima wa Bonde la Bahi 


Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe ametoa wito kwa Wakulima nchini kutumia Ushirika hususan Mfumo wa Stakabadhi ya Ghala kwa lengo la kupata masoko na bei za uhakika.

Wito huo umetolewa wakati wa Kikao na viongozi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Wakulima wa zao la Mpunga wa Bonde la Bahi, Jumanne Juni03, 2020 alipokuwa katika ziara ya kikazi Wilayani Bahi, mkoani Dodoma.

Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda akiongea na Wanaushirika katika ziara ya Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe kwenye Skimu ya Umwagiliaji ya Wakulima wa zao la Mpunga wa Bonde la Bahi 

Naibu Waziri amesema kuwa Serikali ina dhamira ya dhati ya kumuinua mkulima ili anufaike na kilimo chake. Hivyo, ni vyema wakulima kutumia mifumo ya Ushirika pamoja na vituo vya ukusanyaji mazao katika maeneo yao kwaajili ya urahisi wa kufikisha mazao yao katika maghala ya uuzaji kwaajili ya kupata bei yenye tija itakayopatikana kupitia minada rasmi.

Wanaushirika wa Skimu ya Umwagiliaji ya Wakulima wa zao la Mpunga wa Bonde la Bahi wakiwa katika mkutano na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe

Aidha, Naibu Waziri ametoa agizo kwa watendaji kushirikiana na wakulima wa Skimu ya Bahi kujenga Ofisi ya kuhudumia Skimu hiyo ndani ya eneo la Skimu kwa lengo la kuimarisha huduma kwa wakulima na kuboresha kilimo cha umwagiliaji kinachofanyika hivi sasa. Alisema kuwa ni matazamio ya Serikali kuwa suala hilo litakapoteelezwa kwa ufanisi ni dhahiri kuwa litakuwa ni mfano  wa kuigwa katika maeneo mengine ya Skimu kama hiyo. Aliongeza kuwa Ofisi hiyo itasaidia wakulima kupata huduma kwa urahisi kupitia Afisa Kilimo, Afisa Ushirika pamoja na Wataalamu wengine ambao watapatikana katika miradi hiyo.


Wanaushirika wa Skimu ya Umwagiliaji ya Wakulima wa zao la Mpunga wa Bonde la Bahi wakiongea na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe

Naibu Waziri Bashe amewashauri wakulima kutumia nguvu zao kwa pamoja kuboresha mifumo ya Kilimo waliyonayo ili kuongeza tija na ufanisi zaidi katika Kilimo na amewataka wakulima kuchangia maendeleo yao wenyewe kupitia maamuzi yao ya pamoja ya kuchangia kiasi cha mavuno yao kulingana na uzalishaji wa mkulima na kuuza mazao hayo kwa malengo ya kutatua changamoto zinazowakabili. Changamoto hizo ni pamoja na ujenzi wa maghala, kuboresha na kukarabati miundo mbinu ya Skimu za Kilimo.

“Tunaweza kuamua kuhifadhi kwenye ghala gunia mbili za mazao ya mkulima hiki kikiwa ni wastani wa kwa kiwango cha chini na kwa pamoja tukaamua kuyauza mazao hayo kwa mnada wa uwazi ambapo mapato yatakayopatikana yatusaidie wenyewe kuimarisha kilimo chetu,” alisisitiza Bashe.

Katika Kikao hicho Naibu Waziri amewaagiza Viongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Bahi kutenga maeneo maalum ya uuzaji wa mazao ya wakulima wadogowadogo ili kuwa na urahisi kukutana na wauzaji katika hatua za soko la awali, akisisitiza maeneo hayo kuwa na mizani zilizokaguliwa ili wakulima wauze kwa vipimo sahihi na si vinginevyo.

Wanaushirika wa Skimu ya Umwagiliaji ya Wakulima wa zao la Mpunga wa Bonde la Bahi wakiandaa mazao yao kwaajili ya huhifadhi na kuuza

Mhe. Bashe amewataka Viongozi wa Skimu, Viongozi wa Wilaya ya Bahi kushirikiana kwa pamoja na Wadau wa maendeleo pamoja na taasisi za kifedha kuangalia namna bora ya kuongeza thamani ya mpunga huo kwa kuanzisha  kiwanda chenye kinu cha  kukoboa mpunga na hatimaye kuuza mchele. Jambo ambalo wakulima hao waliliunga mkono kutokana na kuongeza ubora wa thamani na kuongeza kipato kwa wakulima.

Pamoja na mambo mengine, Naibu Waziri ameagiza Watendaji wa Wilaya ya Bahi kwa kushirikiana na Serikali  kuratibu zoezi la kuwatambua wakulima kwa lengo la kuanzisha kanzidata ya wakulima pamoja na upatikanaji wa vitambulisho kwa wakulima wa Bonde la mpunga la Bahi. Akifafanua kuwa Skimu hiyo ikawa ni mfano utakaoendelezwa katika maeneo mengine ili kuongeza tija na ufanisi kwa wakulima.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda amemshukuru Naibu Waziri wa Kilimo kwa kufika katika Wilaya hiyo kuona shughuli mbalimbali za Kilimo zinazoendelea Wilayani hapo. Mkuu huyo alipongeza juhudi zinazoendelea hususani za uimarishaji wa Ushirika kwa mfumo wa Stakabadhi ya ghala ambao unaendelea kutekelezwa Wilayani hapo kipindi hiki ambapo minada ya mazao ikiendelea na wananchi wakinufaika na bei za mauzo za minada hiyo.  


No comments:

Post a Comment